Mahakama Kuu ya Kenya imetaja sheria ya kuwazuia Marais wastaafu kujihusisha na siasa kuwa kinyume cha katiba ,ikiwemo kufanya kampeni na kupiga siasa za chama.
Kwenye uamuzi wake wa Jumatatu Septemba 21,Jaji Bahati Mwamuye, alitaja sehemu ya sita inayosimamia malipo ya uzeeni kwa Rais mstaafu kuwa kinyume cha katiba na isiyo na mwelekeo.
Kitengo hicho kinamzuia Rais mstaafu kuwa na afisi yoyote ya chama cha kisiasa miezi sita baada ya kung’atuka afisini.
Uamuzi huo unajiri wakati ambapo kumekuwa na mjadala mkali kuhusu kujihusisha katika siasa kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, huku utawala wa kenya Kwanza ukimshutumu kwa kufadhili upinzani kupinga serikali.
Jaji Lawrence Mugambi mnamo Septemba 14, mwaka huu alidumisha uamuzi wa sehemu ya sita katika katiba ya Kenya unaomzuia Rais mstaafu kumiliki chama cha kisiasa zaidi ya miezi sita baada ya kustaafu.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na kundi la Sheria Mtaani na Shadrack Wambui katika Mahakama ya Kiambu .
Uamuzi huo ni afueni kubwa kwa Rais mstaafu Kenyatta huku likiwa pigo kwa baadhi ya viongozi wanaogemea serikali ambao walitaka kiongozi huyo wa chama cha Jubilee afungiwe kupiga siasa.