Kenya na Panama kuimarisha uhusiano

Mkuu wa Mawaziri na waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Panama, Javier Martínez-Acha Vásquez, mjini New York.

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya inalenga kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na kidiplomasia na Panama huku ikitafuta fursa mpya za kuunganisha Afrika na Amerika Kusini.

Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Musalia Mudavadi, alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Panama, Javier Martínez-Acha Vásquez, mjini New York, ambapo walijadili namna ya kupanua ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Mudavadi alisema mazungumzo hayo yalilenga kuunganisha nafasi ya Kenya kama lango la kiuchumi la Afrika na mitandao ya kimataifa ya usafirishaji na kifedha ya Panama.

Pande hizo mbili pia zilijadili kupanua ushirikiano katika biashara na uwekezaji, masuala ya baharini, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na diplomasia ya kimataifa.

Mazungumzo hayo pia yaligusia mpango wa Panama kufungua Ubalozi wake jijini Nairobi, hatua ambayo itaimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kitaasisi kati ya nchi hizo.

Mudavadi alisema Kenya inajenga madaraja mapya kati ya Afrika na Amerika Kusini ili kufungua njia mpya za biashara, uwekezaji na fursa za kiuchumi.

Alisema ushirikiano imara kati ya Kenya na Panama utasaidia kuunganisha masoko, kuunda fursa kwa wafanyabiashara na vijana wa Kenya, na kupanua ushawishi wa Kenya katika uchumi wa dunia.

Hatua hiyo inajiri wakati Kenya ikiendelea kutafuta ushirikiano wa kimataifa unaolenga kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuunda fursa mpya za kiuchumi.

Share This Article