Utawala wa Trump unaripotiwa kuandaa vikwazo vikali dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ambavyo vinaweza kuvuruga fedha na shughuli za kila siku za mahakama hiyo.
Vikwazo hivyo kutoka Marekani vinalenga kupiga marufuku miamala mingi na ICC baada ya kipindi cha mpito cha miezi sita hadi saba, kulingana na gazeti la The Wall Street Journal.
Shirika la habari la Reuters nalo limeripoti kwamba vikwazo hivyo huenda vikatangazwa hivi karibuni, likinukuu vyanzo viwili vinavyofahamu suala hilo.
Maafisa ambao hawakutaka kutambulishwa walisema uamuzi unaweza kukamilishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York wiki hii au baada yamkutano huo.
Hatua hizo huenda zikawazuia raia na kampuni za Marekani kuipa ICC pesa, bidhaa au huduma bila leseni kutoka Hazina ya Marekani.
Benki na kampuni nyingine mara nyingi huchukua msimamo wa tahadhari kupita kiasi dhidi ya vikwazo vya Marekani kwa sababu zinategemea ufikiaji wa mfumo wa kifedha wa Marekani.
ICC iliundwa mwaka 2002 kushtaki watu wanaoshukiwa kwa mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu wakati mamlaka za kitaifa haziwezi au hazitaki kufanya hivyo.
Uhusiano kati ya Marekani na ICC ulizorota baada ya mahakama hiyo kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.