Mudavadi awataka viongozi kupunguza joto la kisiasa kuelekea 2027

Alisema hayo kwenye hafla ya mchango katika Kanisa la AIC Kapseng’ere, Kaunti ya Nandi.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, amewataka viongozi wa kisiasa kutoka pande mbalimbali kupunguza joto la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Mudavadi ameonya dhidi ya siasa za kikabila, matamshi ya kiholela na juhudi za kudhoofisha demokrasia.

Waziri huyo wa masuala ya kigeni alisema safari kuelekea uchaguzi wa 2027 inapaswa kuongozwa na mawazo, uongozi na kura badala ya siasa za migawanyiko.

Aliwataka viongozi kuipa Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu Mipaka, IEBC nafasi ya kutosha kujiandaa kwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na sajili safi na ya kuaminika ya wapiga kura.

Mudavadi alisema hayo wakati wa hafla ya mchango katika Kanisa la AIC Kapseng’ere, Kaunti ya Nandi.

Mkuu huyo wa Mawaziri alisema ana imani kwamba Rais William Ruto atashinda uchaguzi ujao kwa kiwango kikubwa kupitia uamuzi wa kidemokrasia wa Wakenya, akisisitiza kuwa ushindi huo unapaswa kupatikana kwa njia zinazozingatia Katiba.

Pia aliitaka Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wanasiasa wanaochochea ukabila, kuongeza mivutano au kudhoofisha makusudi imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

Mudavadi alisema nguvu za kisiasa za Nandi hazipaswi kutegemea idadi pekee, bali pia uongozi bora, mawazo na ushawishi mkubwa wa kitaifa.

Aliwahimiza Wakenya kuchagua umoja na demokrasia wakati taifa likijiandaa kwa uchaguzi wa 2027.

Share This Article