Rais William Ruto leo Alhamisi amewaonya wanasiasa dhidi ya kueneza semi za chuki huku taifa hili linapokaribia Uchaguzi Mkuu mwaka 2027, akidokeza kuwa zinaweza sambaratisha umoja wa nchi.
Akiwa kwenye siku ya pili ya ziara yake katika eneo la South Rift, kiongozi huyo wa taifa alitoa wito kwa wanaowania nyadhifa mbali mbali za uongozi, kuuza sera zao kwa njia ya amani.
Ruto aliwanyooshea kidole cha lawana viongozi wa upinzani akiwataja kuwa wanaeneza siasa za migawanyiko badala ya kuwaunganisha Wakenya.
“Watu wa Kernya hawatakubali upinzani kurudisha nyuma taifa hili. Ukosefu wao wa rekodi ya ajenda ya maendeleo kwa taifa hili, ni tisho kwa hatua ambazo tumepiga kama taifa,” alidokeza Rais Ruto.
Kwenye ziara hiyo Rais Ruto alizindua miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kilomita 34 ya Panda Pilis-Kampala/Bokoiyot-Mabasi katika kaunti ya Kericho, akisema kuwa barabara hiyo itaboresha uunganishaji na kurahisisha usafiri wa mazao ya kilimo hadi sokoni.
Aidha, alikabidhi soko la kisasa la Kapkatet katika eneo bunge la Bureti, kaunti ya Kericho kwa Mama Mboga na wafanyabiashara wengine wadogo wadogo. Soko hilo litawahifadhi wafanyabiashara 200.
“Soko hili ni moja kati ya 12 ambazo tunajenga katika kaunti ya Kericho kuhakikisha wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao katika mazingira bora, yaliyo na umeme, maji vyoo, vyumba vya kuhifadhi na mtandao wa inteneti,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto yuko kwenye ziara ya siku nne katika eneo la South Rift ambako atazindua na kukagua miradi ya maendeleo katika kaunti za Bomet na Kericho.