Kenya na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) zimeazimia kuboresha ushirikiano wao kwa manufaa ya raia.
Katibu wa Wizara ya Fedha Dkt. Chris Kiptoo amesifia ushirikiano wa muda mrefu wa zaidi ya miaka 45 iliyopita kati ya pande hizo mbili, akisema umekuwa muhimu katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo vijijini humu nchini.
Alisema mipango mbalimbali ya usaidizi ilitolewa kwa jamii zaidi ya milioni 4.5 katika kaunti 15 wakati wa kipindi hicho.
Dkt. Kiptoo aliyasema hayo alipokutana na Matteo Marchisio, ambaye ni Mkurugenzi mpya wa IFAD humu nchini aliyemtembelea.
“Tunatazamia fursa za ufadhili zaidi wakati tukiimarisha ushirikiano kati ya Kenya na IFAD na kuendeleza mipango ambayo inaboresha mapato na kubuni nafasi za kudumu kwa wakulima na jamii za vijijini,” aliongeza Dkt. Kiptoo.