Jose Chameleone amkomesha Kid Fox

Kid Fox alijifanya kutofahamu wasanii wa kizazi cha sasa na kususia mafanikio ya nyota wakubwa wa muziki.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki nguli wa Uganda Jose Chameleone amemjibu vikali msanii mkongwe wa dancehall Kid Fox, kufuatia kauli zake zenye utata kwa vyombo vya habari aliporejea Uganda baada ya kukaa Japan miaka 15.

Kid Fox, ambaye jina lake halisi ni Steven Kiggundu, alizua hasira kubwa wakati wa ziara yake kwa vyombo vya habari aliporejea nchini humo,ambapo alijifanya kutofahamu wasanii wa kizazi cha sasa na kususa mafanikio ya nyota wakubwa wa muziki, akiwemo mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa, Bobi Wine.

Akijibu kauli hizo, Jose Chameleone aliyekerwa alimshambulia Kid Fox, akimtaja kama mtu anayelenga kupata umaarufu wa bei rahisi na ambaye ametengana na hali halisi ya muziki wa sasa nchini humo.

Chameleone alimkumbusha mwimbaji huyo kwamba tasnia ya muziki nchini Uganda imebadilika kwa kiasi kikubwa wakati wa kutokuwepo kwake kwa muda mrefu.

“Uliondoka ukiwa mfalme, lakini sasa tuna wafalme zaidi ya watano,” Chameleone alisema, huku akipuuza juhudi za Kid Fox kutumia matusi na kejeli kama njia ya kufanikisha kurejea kwake kwenye muziki.

Majibu ya Chameleone yanaungwa mkono na ukosoaji mkubwa kutoka kwa magwiji wengine wa tasnia kama Weasel Manizo na King Saha, ambao wote wamemwonya Kid Fox dhidi ya kudharau wasanii waliobaki nchini na kujenga tasnia hiyo wakati yeye akiwa mbali.

Mashabiki wa muziki nchini pia wamemkosoa Kid Fox mtandaoni, wakimshauri ajikite katika kuimarisha na kuhalalisha kurejea kwake kwenye muziki badala ya kutafuta umaarufu wa bei rahisi kupitia mashambulizi yenye sumu kwenye vyombo vya habari.

Share This Article