Koome atangaza kuanzishwa kwa mahakama mpya za mahakimu

Hatua hiyo inalenga kusongesha huduma za mahakama karibu na Wakenya.

Marion Bosire
2 Min Read
Martha Koome - Jaji Mkuu

Jaji Mkuu Martha Koome ametangaza rasmi kuanzishwa kwa mahakama nne mpya za mahakimu, katika hatua inayolenga kusongesha huduma za mahakama karibu na Wakenya.

Kiongozi huyo wa idara ya mahakama aliratibisha hatua hiyo kupitia chapisho kwenye gazeti rasmi la serikali.

Mahakama hizo mpya ziko Kegonga, Emuhaya, Maara na Tarakwa na zilianza kufanya kazi Septemba 1, 2026, kufuatia notisi hizo za Gazeti Rasmi la Serikali zilizotolewa na Jaji Mkuu mnamo Agosti 26, 2026.

Mahakama ya Hakimu ya Kegonga itakuwa chini ya usimamizi wa Mahakama Kuu ya Migori, huku Mahakama ya Hakimu ya Emuhaya ikiwa chini ya Mahakama Kuu ya Vihiga.

Mahakama ya Hakimu ya Maara imewekwa chini ya usimamizi wa Mahakama Kuu ya Chuka, huku Mahakama ya Hakimu ya Tarakwa ikiwa chini ya Mahakama Kuu ya Eldoret.

Kuanzishwa kwa mahakama hizo ni sehemu ya juhudi za Idara ya Mahakama za kusambaza huduma za mahakama katika maeneo mbalimbali na kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Vituo hivyo vipya vinatarajiwa kupunguza umbali na gharama ambazo wakazi hulazimika kutumia wanaposafiri kufuata huduma za mahakama.

Hatua hiyo inapanua mtandao wa mahakama za chini nchini Kenya na kuimarisha juhudi za Idara ya Mahakama kuhakikisha haki inapatikana kwa urahisi, kwa ufanisi na kwa wakati kwa watumiaji wa mahakama kote nchini.

Share This Article