Mjasiriamali na msanii wa Tanzania, Hamisa Mobetto, amefanywa kuwa bingwa wa Kimataifa wa UNESCO.
Sasa anachukua nafasi mpya inayolenga kuhamasisha usalama wa kidijitali na matumizi ya uwajibikaji ya teknolojia miongoni mwa vijana.
Uteuzi huo ulitangazwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari pamoja na UN Youth Masterclass jijini Dar es Salaam, Agosti 28, 2026.
Kupitia ushirikiano na UNESCO Tanzania na wakfu wa mrembo huyo uitwao, Mobetto Foundation, atahamasisha uelewa wa vyombo vya habari na taarifa, matumizi salama ya teknolojia, pamoja na usalama wa kidijitali, hususan kwa wanawake na wasichana.
Hamisa Mobetto amesema nafasi hiyo ina umuhimu mkubwa kwake binafsi, kutokana na kuwa amewahi kukumbana na unyanyasaji mtandaoni, taarifa za uongo na ukatili wa kijinsia unaofanyika kupitia mtandao.
Anatarajia kutumia jukwaa lake kuwasaidia vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kujilinda dhidi ya madhara ya mtandaoni.
Uteuzi wake unaashiria hatua mpya katika juhudi zake za utetezi, akilenga kusaidia kujenga mazingira ya kidijitali yaliyo salama na yenye kuwawezesha vijana wa kizazi kijacho.
Haya yanajiri siku chache baada ya Mama huyo wa watoto wawili kulalamikia ongezeko la visa vya unyanyasaji mitandaoni akielezea aliyoyapitia yeye mwenyewe.
Lalama za Hamisa ziliwafikia wengi akiwemo Mheshimiwa Dorothy Gwajima aliyetoa tamko kali la kumuunga mkono Mobetto na kulaani unyanyasaji unaoendelea mtandaoni unaomlenga yeye pamoja na familia yake.