Rais wa muda wa Venezuela, Delcy Rodriguez, amesema nchi hiyo inasalia na uhuru wake licha ya tangazo kwamba itakabidhi haki za mabilioni ya mapipa ya mafuta yake kwa Marekani.
Makubaliano hayo ya kihistoria na Washington ya kukabidhi haki za mapipa bilioni 65 ya mafuta ya Venezuela, yatadumu miaka 25 na kuiwezesha Venezuela kuendeleza sekta yake ya mafuta.
Wakati huo huo, itaendelea kuhifadhi umiliki na uhuru wa rasilimali zake, Rodriguez alisema katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja kwenye televisheni jana Jumamosi.
Alisema mradi huo unalenga kuendeleza maeneo 17 ya kimkakati ya uzalishaji wa mafuta, huku lengo la awali likiwa kuzalisha mapipa milioni 1.5 kwa siku.
Mpango mpana zaidi pia unajumuisha uendelezaji wa vitalu vinane vipya vya mafuta ambavyo havijawahi kuchimbwa, ikiwa ni sehemu ya upanuzi mpana wa sekta ya nishati nchini humo.
Chini ya makubaliano hayo, dola 19 kutoka kwa kila pipa la mafuta litakalozalishwa na kuuzwa Marekani zitaelekezwa Caracas, mpango unaoweza kuiingizia Venezuela hadi dola bilioni 209 kwa mwaka, kwa kutegemea bei ya mafuta, kulingana na Rodriguez.
“Venezuela itaendelea kumiliki rasilimali zake za asili huku ikitumia mtaji, teknolojia na utaalamu wa uendeshaji kusaidia kufufua sekta ya kimkakati ambayo imeathiriwa sana na vikwazo”, alisema Rais huyo.
Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mipango ya nchi hiyo kuchukua udhibiti wa sehemu ya akiba kubwa ya mafuta ya Venezuela.
Makubaliano hayo yatawezesha kampuni za kigeni, zikiwemo kampuni za Marekani, kusaidia kuokoa miundombinu ya nishati ya Venezuela iliyoharibika.
Caracas imekuwa ikishinikizwa kutekeleza matakwa ya Washington tangu Januari, baada ya vikosi maalum vya Marekani kumteka aliyekuwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na kukabidhi uongozi kwa makamu wake wa rais, Rodriguez.