Rais William Ruto ametoa onyo kali kwa wanaotumia vijana kusababisha vurugu katika mikutano ya kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini.
Ruto amesema hulka hiyo haitavumiliwa abadan nchini, ikiwa imesalia takriban mwaka mmoja kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
“Katika miezi ya hivi karibuni, tumeshuhudia wasiwasi unaoongezeka wa matumizi ya magenge na vijana, wanaosafirishwa na kulipwa ili kuvuruga mikutano ya kisiasa, kutishia wapinzani na kusababisha vurugu,” alisema Rais Ruto leo Ijumaa wakati wa hafla ya kufuzu kwa makurutu wa polisi huko Kiganjo, kaunti ya Nyeri.
“Wacha niwe bayana zaidi kuhusu hili: Vurugu zinazochochewa kisiasa hazina nafasi katika demokrasia yetu. Kwa hivyo, Huduma ya Taifa ya Polisi na asasi zetu zote za usalama zinapaswa kuchukua hatua thabiti, ya kisheria na isiyopendelea upande wowote dhidi ya yeyote anayefadhili, kupanga au kuchochea vurugu za kisiasa.”
Matamshi yake yanakuja wakati serikali imetakiwa kuchukua hatua dhidi ya wahuni ambao wamekuwa wakitumiwa yamkini na wanasiasa kusababisha vurugu katika mikutano ya kisiasa nchini.
Vurugu za hivi karibuni kushuhudiwa nchini zilitokea katika kaunti ya Homa Bay wakati wa mkutano wa vuguvugu la Linda Mwananchi kiasi cha kuwalazimisha viongozi wa vuguvugu hilo kutumia vichochoro kufika eneo la mkutano.
Hudumaya Taifa ya Polisi, NPS imesema washukiwa zaidi ya 30 wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo wakati uchunguzi ukiendelea.
Vurugu zingine zilishuhudiwa hasa wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.