Tom Byabagamba aliyekuwa mlinzi wa Rais Rwanda afariki

Alikamatwa mwezi Agosti mwaka 2014 kuhusiana na makosa ya kuchochea uasi dhidi ya serikali na kuchafua taswira ya serikali

Marion Bosire
2 Min Read

Kanali wa zamani wa Rwanda, Tom Byabagamba, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa kikosi maalum cha ulinzi wa Rais Paul Kagame, amefariki akiwa na umri wa miaka 59, gerezani alikokaa kwa takribani miaka 12.

Byabagamba alikamatwa mwezi Agosti mwaka 2014 baada ya kuhudumu katika ulinzi wa karibu wa Rais Kagame na baadaye kuwa mkuu wa Republican Guard, kikosi kinachohusika na ulinzi wa Rais na maeneo muhimu ya serikali.

Mwaka 2016, mahakama kuu ya kijeshi nchini Rwanda ilimhukumu kifungo cha miaka 21 baada ya kupatikana na hatia katika makosa yaliyohusisha kuchochea uasi dhidi ya serikali na kuchafua taswira ya serikali.

Hukumu hiyo ilipunguzwa hadi miaka 15 na mahakama ya rufaa mwaka 2019.

Taarifa za kifo chake zilitangazwa na ndugu yake, David Himbara, ambaye ni mshauri wa zamani wa Rais Kagame na mkosoaji wa serikali ya Rwanda aliye uhamishoni.

Familia haijataja sababu ya kifo, huku mamlaka za Magereza na serikali ya Rwanda zikiwa hazijatoa maelezo ya wazi kuhusu mazingira ya kifo hicho.

Kesi ya Byabagamba imekosolewa sana na mashirika ya haki za binadamu, huku Human Rights Watch ikiielezea kesi hiyo kuwa na dosari na kutaja madai mazito yaliyohusisha mateso na kuingiliwa kwa mashahidi.

Kifo chake kinakuja takriban mwaka mmoja unusu baada ya kifo cha gerezani cha Brigedia Jenerali Mstaafu Frank Rusagara, ambaye alihukumiwa pamoja na Byabagamba.

Share This Article