Nchimbi avuliwa uanachama wa CCM

Kamati kuu ya chama ilifanya kikao jana na kuafikia uamuzi huo.

Marion Bosire
2 Min Read

Makamu wa Rais aliyejiuzulu nchini Tanzania Emmanuel John Nchimbi, sio mwanachama wa chama tawala nchini humo CCM.

Hatua hii inafuatia kikao cha halmashauri kuu ya CCM kilichofanyika jana, Agosti 26, 2026, chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kikao hicho, Katibu Mkuu wa chama hicho Asha Roze Migiro alitoa tangazo kwamba halmashauri kuu ya chama ilijadili suala la nidhamu na maadili linalomkabili Nchimbi na kuthibitisha kwamba kanuni zilikiukwa.

“Kamati Kuu imejadili kuhusu suala la nidhamu na maadili ambalo lilikuwa linamkabili Emmanuel Nchimbi, na baada ya kuzingatia taarifa zote zilizokuwepo ilithibitika kwamba katiba ya CCM na kanuni zake zilikiukwa, na hivyo Nchimbi amefukuzwa uanachama,” alisema Migiro.

Dkt. Emmanuel John Nchimbi alijiuzulu Agosti 25, 2026, na katika barua ya kufahamisha umma, alielezea kwamba alimwandikia Rais barua ya kuomba kujiuzulu kwa sababu anaamini kwamba Rais alihitaji mabadiliko katika wadhifa huo na alikuwa amemuahidi kwamba atatumika hadi wakati Rais atataka mabadiliko.

Kabla ya hapo kulikuwa na taarifa za kutoelewana kati ya Nchimbi na Rais Samia, ripoti zilizosababisha gazeti moja nchini humo kufungiwa kwa muda wa miezi sita.

Nchimbi alitangaza pia kwamba ameacha siasa kabisa pamoja na utumishi wa umma kumaanisha amestaafu.

Kati ya masuala ambayo amekuwa akisisitizia Watanzania ni katiba mpya ambapo amekuwa akiwahimiza wapambane wapate katiba mpya.

Share This Article