Mwanamuziki nguli kutoka Uganda Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleone, atatumbuiza kwenye tamasha ya Jumamosi ya msanii wa Kenya Redsan.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Jose amethibitisha uwepo wake siku hiyo, rafiki yake atakapokuwa akisherehekea miaka 30 katika tasnia ya muziki.
“Ndugu yangu REDSAN, Rafiki, Familia!! Hadithi yetu haiishi! Ninataka nikushukuru kwa kunikaribisha Kenya, kunifahamisha kwa familia yako kubwa !! Eastleigh, Dandora, South B, South C! Kibera, Kayole na sehemu nyingine nyingi!!!” aliandika Chameleone.
Aliendelea kwa kusimulia jinsi Redsan alimpeleka klabu cha burudani cha Florida 2000, akisema wakati huo walikuwa wakiota kuhusu siku kama hizi na zimefika.
Chameleone alitumbuiza pia kwenye tamasha ya kusherehekea miaka 25 katika tasnia ya muziki ya mwanamuziki wa Kenya Nameless.
Urafiki kati ya Jose Chameleone na Redsan ulianza kunako mwaka 1998, Chameleone alipohamia Kenya na kuanza kufanya kazi chini ya kampuni ya Ogopa Deejays ambapo Redsan alikuwa.
Usuhuba wao ulitiwa shime na hatua ya Redsan ya kumsaidia Chameleone kuimba wimbo “Bageya” uliosaidia katika kuwapa umaarufu wawili hao katika eneo zima la Afrika mMashariki.
Tamasha ya Redsan@30 itaandaliwa Jumamosi Agosti 29, 2026 katika uwanja wa Carnivore jijini Nairobi ambapo wasanii kadhaa watatumbuiza kama vile Akothee, Bebe Cool wa Uganda, AY wa Tanzania na wengine wengi.