Dolly Parton ameaga dunia

Mwakilishi wake alielezea kwamba alifariki kwa amani huko Nashville baada ya kuugua saratani kwa muda mfupi

Marion Bosire
2 Min Read

Dolly Parton, mwimbaji mashuhuri wa muziki wa country, mtunzi wa nyimbo, mwigizaji na mfadhili, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80, haya ni kulingana na tangazo kutoka kwa familia yake.

Kwa mujibu wa mwakilishi wake, Dolly alifariki kwa amani huko Nashville baada ya kuugua saratani kwa muda mfupi.

Parton, aliyezaliwa Tennessee mwaka 1946, alijenga kazi iliyotukuka zaidi katika historia ya muziki maarufu. Sauti yake ya kipekee na umahiri wake wa kutunga nyimbo vilizaa nyimbo maarufu kama Jolene, Coat of Many Colors, 9 to 5 na I Will Always Love You.

Mbali na muziki, Parton alijulikana duniani kote kwa ukarimu wake na shughuli zake za kibiashara.

Kupitia mpango wake wa Imagination Library, alisaidia kukuza usomaji wa watoto kwa kuwapatia vitabu bila malipo. Pia alikuwa mtu muhimu katika tasnia ya burudani kupitia uigizaji na bustani yake ya burudani ya Dollywood.

Parton aliendelea kufanya kazi na kuhamasisha mashabiki hadi katika miaka yake ya baadaye, licha ya changamoto za kiafya za hivi karibuni.

Kifo chake kimeibua maombolezo na salamu za rambirambi kutoka kwa mashabiki, wanamuziki, waigizaji na viongozi mashuhuri duniani kote.

Akiwa na kazi iliyodumu zaidi ya miongo sita, Parton ameacha urithi mkubwa wa muziki pamoja na sifa ya upendo, ucheshi na kujitolea kwa jamii.

Kwa mamilioni ya mashabiki wake, nyimbo zake na kazi zake za kibinadamu zitaendelea kuathiri na kuhamasisha vizazi vijavyo.

Share This Article