Maafisa 2 zaidi wafikishwa kortini sakata ya PROFIT

Martin Mwanje
3 Min Read
Washukiwa Eric Otieno Achila na Susan Wangari

Maafisa wawili zaidi wa Wizara ya Fedha wamefikishwa mahakamani kwa madai ya ufujaji wa hadi shilingi bilioni 1.5 za Mpango wa Upelekaji wa Uvumbuzi na Teknolojia Mashinani (PROFIT). 

Mpango huo unatekelezwa na Wizara ya Fedha kwa ufadhili kutoka kwa Mfuko wa Kimataifa wa Ustawi wa Kilimo (IFAD).

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) anasema wawili waliofikishwa mahakamani ni Eric Otieno Achila ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Dangzerina Enterprises na Susan Wangari ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Maxtor Supplies and Graybar Distributors.

Wawili hao walifikishwa mbele ya Harrison Barasa Omwima wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi jijini Nairobi wakikabiliwa na mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya ulaghai.

Wote hao walikanusha mashtaka hayo huku akiachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 1.5 na mdhamini wa kiasi kama hicho au elfu 650 pesa taslimu.

Wangari aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 1.5 na mdhamini wa kiasi kama hicho au elfu 700 pesa taslimu.

Wawili hao ni sehemu ya kundi la maafisa kutoka Wizara ya Fedha wanaotumiwa kwa kubadhiri shilingi bilioni 1.5 za mpango huo.

Wiki jana, maafisa 9 waliokamatwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC walifikishwa mbele ya Hakimu Rose Ndobi wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi jijini Nairobi kwa madai ya ubadhirifu wa fedha za umma wakikabiliwa na mashtaka 121.

Waliofikishwa mahakamani ni Nemwel Moturi Motanya (Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu, Wizara ya Fedha), John Ngure Kabutha (Mratibu wa Mpango wa PROFIT), John Maina Muriithi (Mhasibu Mwandamizi, Wizara ya Fedha), Gladys Juliet Oroni (Mwasisi wa kampuni za Mawindo Enterprise, Brigs Agencies na Green Basils Agencies) na Brian Kiprop Chepkarat (Mwasisi wa Kampuni ya El Konyinta Technologies).

Wengine ni Ian Kwemoi Chepkarat (Mkurugenzi wa kampuni za 020 Investments Ltd na Vidi Vici Ltd), James Omwodo Ndai (Mwasisi wa kampuni za Ednas Agencies, Prozzep Technologies na Steeren Entreprises), Jimmy Carter Odoyo Osodo (Mwasisi wa kampuni ya Cadnic Investments) na Josphat Kamau Kamoshe (Mkurugenzi wa kampuni ya Blue Dart Agencies Ltd).

Wote hao walikana mashtaka na kesi dhidi yao itatajwa tena Septemba 2 mwaka huu.

Awali, EACC iliwataka washukiwa wengine kwenye sakata hiyo kufika katika makao makuu ya EACC jijini Nairobi kuhusiana na sakata hiyo.

Share This Article