Rais Ruto azindua miradi ya maendeleo Narok

Miradi inayozinduliwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na usambazaji wa umeme kwa wakazi wa eneo hilo.

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ametua katika kaunti ya Narok ambako ameanza ziara ya maendeleo ya siku mbili leo Jumanne. 

Mapema hii leo, Ruto alizindua ujenzi hadi kuwekwa lami wa barabara ya Enengetia – Olpusimorru huko Narok Kaskazini, kaunti ya Narok.

Akiwahutubia wakazi, Rais alielezea ujenzi mbalimbali wa barabara unaoendelea eneo hilo kwa ajili ya kuboresha usafirishaji wa watu na bidhaa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kadhaa katika eneo la Narok Mashariki.

Aidha, alielezea nia ya serikali yake kuhakikisha wakazi wanapata umeme.

“Leo leo, naenda pia kupanga mambo ya stima, kwa sababu nimeambiwa ya kwamba bado kuna wananchi wengi hawajafikiwa na stima makwao,” alisema Rais Ruto.

“Tumetoa pesa ya serikali 2.8 bilion ya mambo ya stima ya Narok County. Na leo mimi naenda kuzindua hiyo mpango ndio tuhakikishe ya kwamba tunasukuma stima ifike kwa manyumba ya wananchi.”

Kiongozi wa nchi amekuwa akizuru maeneo mbalimbali nchini kuzindua miradi ya maendeleo, na hivi maajuzi alitembelea kaunti ya Taita Taveta alikozindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

 

Share This Article