Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu anatarajiwa kuendelea kujitetea mahakamani leo, katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Hii ni baada ya jopo la majaji watatu linalosikiliza kesi hiyo kuamua Ijumaa kwamba ana kesi ya kujibu.
Siku hiyo Lissu alipatiwa nafasi ya kuanza kutoa ushahidi wake wa utetezi ambapo aliamua pia kwamba atajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, bila kuhusisha mawakili.
Orodha aliyowasilisha mahakamani ya mashahidi ambao angependa kuwaita kizimbani ilishangaza wengi Ijumaa kwani ilijumuisha Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mstaafu Philip Mpango na Waziri Mkuu Mstaafu Kassim Majaliwa.
Alitaja pia viongozi wa CHADEMA kama John Heche, John Mnyika, Amani Golugwa na Brenda Rupia.
Hata hivyo, serikali ilipinga kuitwa kwa viongozi wakuu wa Serikali kama Rais mahakamani kutoa ushahidi. Upande wa utetezi umepinga hoja hiyo, ukisisitiza kuwa sheria inaruhusu mtu yeyote kuitwa kutoa ushahidi mahakamani.
Tundu Antiphas Mughwai Lissu, amekuwa kizuizini tangu Aprili 9, 2025 alipokamatwa kufuatia kampeni aliyokuwa akiendesha ya kuhimiza mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Hatua hiyo ilichukuliwa kama uchochezi wa raia kususia uchaguzi ndiposa akafikishwa mahakamani Aprili 10, 2025 na kushtakiwa kwa uhaini.
Upande wa serikali katika kesi hiyo ulikuwa umeorodhesha mashahidi 30 lakini waliofikishwa mahakamani ni mashahidi 17, wa 18 akikosa kufika mahakamani kutokana na kile kilichotajwa kuwa dharura ya kiafya.