Mwanawe mwanamuziki wa Uganda Jose Chameleone, Abba Marcus amezungumza kwa mara ya kwanza tangu kuachiliwa kutoka rumande alikokaa kwa siku tatu nchini Marekani.
Marcus wa umri wa miaka 20 sasa ametumia mitandao ya kijamii kusema kwamba anatambua amefanya makosa na amejitolea kubadilika na kuwa bora.
“Ninajifunza kutokana na hili na nimejitolea kuwa bora,” alisema msanii huyo anayeishi Marekani huku akiomba umma uheshimu ufaragha wake na mpenzi wake.
Alikamatwa na Polisi wa Edina Agosti 14, 2026, na kupelekwa katika kituo cha Hennepin kabla ya kufikishwa mahakamani Jumatatu Agosti 17, 2026 na sasa anakabiliwa na shtaka moja la shambulio la nyumbani la kiwango cha kosa dogo.
Kesi hiyo inahusishwa na mzozo unaoendelea kati yake na mpenzi wake mjamzito, Angelica Becker, anayejulikana mitandaoni kama Angel.
Mwezi Mei, Angel alimtuhumu Marcus kwa kumshambulia kimwili, madai ambayo Marcus aliyakanusha wakati huo.
Kulingana na taratibu na adhabu za mahakama, kijana huyo angeachiliwa kwa dhamana ya kati ya shilingi elfu 776,220 na shilingi milioni 1.3 lakini mahakama iliamuru aachiliwe kwa masharti bila kulipa dhamana ya fedha.
Masharti ya kuachiliwa kwake hayakuwekwa wazi hadharani.
Ni muhimu kutambua kuwa tuhuma za shambulio la nyumbani bado hazijathibitishwa, na Marcus hajapatikana na hatia ya kosa lolote. Anachukuliwa kuwa hana hatia hadi pale mahakama itakapothibitisha vinginevyo.