Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hii leo amekuwa mwenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.
Mapokezi hayo yamefanyika mapema leo katika Ikulu ndogo ya Zanzibar ambapo Rais Tshisekedi alionekana kwenye picha akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili.
Baadaye viongozi hao wawili waliongoza jumbe zao kwa majadiliano yanayoaminika kuwa kuhusu ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
Rais Tshisekedi amekuwa Nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia jana Agosti 17 hadi leo Agosti 18, 2026, kufuatia mwaliko wa Rais Samia.
Katika taarifa yake baada ya mkutano, Rais samia alielezea kwamba mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na DRC, hususan katika kuziunganisha kupitia ujenzi wa miundombinu, kukuza biashara kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, kuboresha huduma za mipakani na kuwezesha ushiriki zaidi wa sekta binafsi katika shughuli za maendeleo.
Rais Samia alisema kwamba Tanzania ina fursa kubwa katika uzalishaji wa bidhaa za kilimo, uvuvi na mifugo, huku akiikaribisha DRC kutumia fursa hizo katika kuongeza biashara na Tanzania.
Aidha, alisema walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta ya madini, kuanzia uchimbaji, uongezaji thamani na masoko hadi tafiti na kubadilishana uzoefu na ujuzi, ikiwemo kupitia Kituo cha Madini cha Tanzania.
“Tumesisitiza pia umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika masuala ya amani na usalama, kwa lengo la kuimarisha utulivu na ustawi wa wananchi wa Tanzania, DRC na ukanda wetu kwa ujumla,” alimalizia Rais Samia.