Bunge kuunga mkono mabadiliko ya sekta ya afya

Spika Moses Wetang’ula, amesema sheria imara, usimamizi na uwajibikaji ni muhimu kufanikisha Huduma ya Afya kwa Wote.

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge limethibitisha tena dhamira yake ya kuunga mkono mageuzi yanayoendelea katika sekta ya afya nchini Kenya.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amesema sheria imara, usimamizi na uwajibikaji ni muhimu katika kufanikisha Huduma ya Afya kwa Wote.

Akizungumza katika Kongamano la Afya la Kenya mwaka 2026 jijini Nairobi Jumanne, Wetang’ula alisema Bunge lina nafasi muhimu katika kutunga sheria, kugawa rasilimali na kusimamia sekta ya afya.

Alitaja sheria nne kuu zilizopitishwa mwaka 2023 zinazohusu huduma ya afya ya msingi, ufadhili wa vituo vya afya, afya ya kidijitali na bima ya kijamii ya afya.

Alisema mageuzi hayo yanalenga kushughulikia changamoto za muda mrefu, ikiwemo gharama za matibabu, huduma za dharura na ugumu wa kupata huduma za afya.

Wetang’ula alisema Wakenya wapatao milioni 30 sasa wamesajiliwa chini ya mfumo mpya wa bima ya afya, ikilinganishwa na takriban milioni nane chini ya NHIF.

Alitoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi dhidi ya ufisadi na ubadhirifu, ikiwemo madai ya ulaghai na vituo hewa, huku akiunga mkono matumizi ya teknolojia na akili bandia kubaini matumizi mabaya ya fedha.

Pia alitaka wahudumu wa afya wasambazwe kwa usawa na kupatiwa kipaumbele kwa huduma za kinga.

Rais William Ruto alisema familia zaidi ya milioni tisa zimefikiwa na Wahamasishaji wa Afya, huku Wakenya milioni nane tayari wakipokea huduma kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii.

Waziri wa Afya Aden Duale alisema serikali inawekeza katika afya ya kidijitali, huduma maalumu na vifaa tiba, huku ikipanga kuajiri wauguzi na wakunga 5,000.

Mkutano huo unalenga kuimarisha huduma za afya zinazowajibika, zinazopatikana kwa urahisi na zinazomudu gharama nchini kote.

Share This Article