Uchaguzi haupaswi kuwa suala la kufa kupona, ahimiza Ruto

Martin Mwanje
2 Min Read

Mojawapo wa sababu ambazo zimefanya Kenya kutofikia upeo wa maendeleo ni suala la kutoa kipaumbele kwa uchaguzi badala ya kufikiria masuala ya maendeleo na vizazi vijavyo. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ruwaza 2060 katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC, Rais Ruto ameonya kuwa siasa hazipaswi kuwa suala la kufa kupona.

“Kenya ni kubwa kuliko uchaguzi wowote. Kwa muda mrefu, tumefanya uchaguzi uonekane kana kwamba ni suala la kufa kupona. Si hivyo. Sababu ambayo imefanya hatujafikia baadhi ya malengo yetu ni kwa sababu tumefanya mipango yetu si kwa kuzingatia siku zijazo, si kwa kufikiria kizazi kijacho, lakini kwa kufikiria tu uchaguzi ujao,” alisema Rais Ruto.

“Uchaguzi ujao utafanyika na kumalizika, lakini Kenya sharti ifikirie juu ya kipindi cha baada ya uchaguzi. Ni lazima tufikirie juu ya kizazi kijacho,” alisema Rais Ruto.

Rais alielezea kwamba ni kwa sababu anatilia maanani mustakabali wa taifa ndiposa ameamua kuanzisha mjadala kuhusu maendeleo ya taifa baada ya kukamilika kwa Ruwaza 2030 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, licha ya kushauriwa kuwa anapaswa kuzingatia uchaguzi ujao utakaofanywa mwezi Agosti mwakani.

Alisema Kenya itapiga hatua kimaendeleo ikiwa tu siasa zitawekwa kando na jitihada zote kuwekwa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

 

 

Share This Article