Akothee ataka maoni ya kujenga kuhusu huduma za KQ

Amewataka abiria kuacha ukosoaji wa jumla na badala yake kubainisha maeneo makhususi wanakokumbana na changamoto.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya na mtaalamu wa Rasilimali Watu Esther Akoth Kokeyo, maarufu kama Akothee, amewataka abiria wa kampuni ya usafiri wa ndege Kenya Airways, KQ, kutoa maoni ya kujenga kuhusu wanayoyapitia na kuyaona wanapotumia huduma za KQ.

Katika chapisho lake kwenye Facebook, Akothee alisema amepitia maoni kuhusu malalamiko yanayoendelea kuhusu huduma kwa wateja katika Kenya Airways, na kuwataka abiria kuacha ukosoaji wa jumla na badala yake kubainisha maeneo makhususi wanakokumbana na changamoto.

Aliwaomba wasafiri kueleza uzoefu wao kuhusu tiketi na kuhifadhi viti, mawasiliano wanapochelewesha au kufutwa kwa safari, ukaguzi na upandaji wa ndege, utunzaji wa mizigo, huduma ndani ya ndege, weledi wa wahudumu wa ndege, huduma kwa wateja, kushughulikia malalamiko, kurejeshewa fedha na huduma za uaminifu kwa wateja.

Kulingana na Akothee, kurekodi matukio makhususi kutasaidia kubaini mapungufu yanayojirudia katika huduma na kuwezesha kupatikana kwa suluhisho.

Alisema nia yake ni kukusanya malalamiko ya abiria na kuyawasilisha kwa Kenya Airways kwa njia iliyopangwa.

Akothee alisisitiza kuwa suala hilo halipaswi kugeuka kuwa mzozo kati ya shirika hilo na wateja wake, bali liwe fursa ya kuboresha huduma.

Alisema kuridhika kwa wateja ni muhimu kwa mafanikio ya biashara, akiwataka abiria kubadilisha malalamiko yao kuwa maoni ya kujenga yatakayosaidia kuboresha safari zao za baadaye.

Share This Article