Mwanamuziki wa Uganda Kalifah AgaNaga analaumu kampuni ya vyakula KFC, kwa kukiuka hakimiliki zake akidai Sh milioni 550 kutokana na matumizi yasiyoidhinishwa ya muziki wake kwenye matangazo ya kampuni hiyo kwenye mitandao ya kijamii.
Kupitia mawakili wake, Elgon Advocates, Kalifah ameindikia KFC waraka kuhusu ukiukaji wa hakimiliki na haki zinazohusiana na hakimiliki, kufuatia matumizi ya wimbo wa ‘Nassanga Remix’ kwenye video ya matangazo iyochapishwa kwenye akaunti rasmi ya kampuni hiyo ya TikTok.
Mawakili hao wanadai kuwa uzalishaji upya na kuwasilisha wimbo huo kwa umma kwa madhumuni ya kibiashara bila idhini ni ukiukaji wa moja kwa moja wa haki za hakimiliki za mteja wao.
Kulingana nao, jambo hilo linampa haki ya kudai fidia, sehemu ya faida iliyopatikana pamoja na amri ya mahakama ya kuzuia matumizi hayo chini ya Kifungu cha 46 cha Sheria ya Hakimiliki na Haki Zinazohusiana.
KFC imetakiwa kuondoa na kufuta mara moja video hiyo inayodaiwa kukiuka hakimiliki kutoka kwenye akaunti yake ya TikTok na majukwaa mengine yote rasmi ya mitandao ya kijamii ambako huenda video hiyo ilichapishwa.
Imetakiwa pia kusitisha mara moja na matumizi zaidi yasiyoidhinishwa ya kazi za muziki za Kalifah katika matangazo na vifaa vyake vya kibiashara.
Mbali na kuondolewa kwa maudhui hayo, mawakili hao wanadai Sh milioni 500 kama fidia kwa matumizi ya kibiashara ya kazi yake bila idhini, kupotea kwa mapato ambayo angeweza kupata kupitia leseni, pamoja na kuathirika kwa chapa yake.
Mawakili hao pia wanadai Sh milioni 50 za gharama za kisheria zilizotumika katika kushughulikia suala hilo.
KFC imepatiwa siku saba kutekeleza matakwa hayo, la sivyo, Kalifah atalazimika kuanzisha hatua rasmi za kisheria dhidi ya kampuni hiyo.