DCI yamhusisha Gachagua na washukiwa wa mauaji ya Victoria Mutiso

Anadaiwa kuwasiliana na watu wawili wanaohusishwa na mauaji ya daktari Victoria Mutiso.

Marion Bosire
1 Min Read

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI imedai kwamba aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, anawasiliana na watu wawili wanaohusishwa na mauaji ya daktari Victoria Mutiso.

Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa, Agosti 7, Mkurugenzi wa DCI, Mohamed Amin, alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwepo kwa mawasiliano kati ya Gachagua na mmoja wa washukiwa wakuu.

Mkuu huyo wa DCI aliongeza kuwa wachunguzi pia walipata ushahidi unaoonyesha kuwa aliyekuwa Naibu Rais alikuwa akiwasiliana na mwendesha bodaboda aliyewasafirisha washukiwa wa mauaji hayo.

Hata hivyo, akijibu madai hayo wakati wa uzinduzi wa chama cha Democracy for Citizens Party, DCP huko Kiambu, Gachagua alikanusha kuwasiliana na yeyote kati ya washukiwa.

Gachagua alisisitiza kuwa taarifa zake hutoka kwa watu waliomo ndani ya vyombo vya usalama na sio wahusika na mauaji hayo.

Kauli za Amin zilikuja wakati DCI ilitoa taarifa ya kina kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Mutiso, ikisema kuwa wapelelezi wamepiga hatua kubwa kupitia uchunguzi wa kisayansi na operesheni za kijasusi.

Kwa mujibu wa Amin, wapelelezi wamemtambua mtu anayedaiwa kuratibu njama ya mauaji hayo, mwendesha bodaboda aliyemsafirisha mshambuliaji mwenye bunduki, pamoja na watu wengine kadhaa wanaoaminika kushiriki katika kupanga na kutekeleza shambulio hilo.

Share This Article