Mwanamitandao auawa Mexico

Cesar Gastelum alipigwa risasi na kuuawa Jumanne katika mji wa Culiacan, jimbo la Sinaloa nchini Mexico.

Marion Bosire
2 Min Read

Mshawishi wa mitandao ya kijamii kutoka Mexico aliyekuwa na wafuasi 650,000 kwenye TikTok ameuawa alipokuwa akifanya matangazo ya moja kwa moja, haya ni kulingana na mamlaka nchini humo.

Cesar Gastelum alipigwa risasi na kuuawa Jumanne katika mji wa Culiacan, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Sinaloa nchini Mexico, ambalo limekumbwa na machafuko ya uhalifu.

Tukio hilo lilitokea karibu na ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo hilo.

Video ya tukio la kifo cha Gastelumcinaonyesha akiwa anacheka pamoja na wanaume wengine wawili katika maegesho ya magari ya mgahawa wa KFC, wakati wanaume wawili waliwasili kwa pikipiki.

Mmoja wao alionekana akitoa bastola na kumpiga risasi Gastelum, kisha washambuliaji hao wanatoroka eneo la tukio.

Jimbo la Sinaloa limeathiriwa vibaya na mapigano kati ya magenge mawili ya uhalifu ya Sinaloa, Los Mayos na Los Chapitos.

Miili ya watu waliouawa imekuwa ikipatikana katika maeneo mbalimbali ya jiji ikiwa imeachwa na alama zinazotambulisha kundi husika.

“Lazima tufahamu kwa nini mauaji haya ya kusikitisha yalitokea,” Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano na wanahabari uliofanyika Jumatano asubuhi.

“Waliohusika lazima wakamatwe,” aliongeza.

Gastelum alikuwa akichapisha maudhui ambayo ndani yake alijiita “belico”, neno linalotumiwa katika baadhi ya tamaduni ndogo nchini Mexico kuashiria uhusiano au kuhusishwa na utamaduni wa makundi ya uhalifu wa dawa za kulevya.

Baraza la Usalama la Mexico pamoja na waendesha mashtaka wa eneo hilo walisema uchunguzi bado unaendelea, na kwamba inaonekana Gastelum alikuwa amechapisha baadhi ya video ambazo “zilikuwa zikirejelea kundi moja la uhalifu uliopangwa.”

Haya ndiyo mauaji ya pili yaliyotekelezwa wakati wa matangazo ya moja kwa moja baada ya mshawishi wa masuala ya urembo mwenye umri wa miaka 23, Valeria Marquez, kupigwa risasi na kuuawa alipokuwa akifanya matangazo ya moja kwa moja kwenye TikTok katika jimbo la Jalisco, katikati mwa Mexico, Mei, 2025.

Share This Article