Mkurugenzi wa taasisi ya elimu akamatwa kwa kutoa vyeti bandia

Mshukiwa huyo atafunguliwa mashtaka ya kutenegeneza stakabadhi bandia kinyume na sehemu ya 347(a) ya katiba ya Kenya.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mkurugenzi wa taasisi ya elimu akamatwa kwa kutoa vyeti bandia.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu, amekamatwa kwa madai ya kutoa vyeti bandia vya elimu,mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu.

Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), hatua hiyo ilisababisha mwathiriwa mmoja kuachishwa kazi, kutokana na cheti bandia cha elimu alichopewa na mshukiwa huyo.

Philip Kipsoi Kiyeng, Mkurugenzi wa Taasisi ya elimu ya Region Group College,alikamatwa Eldoret mjini baada ya Tume ya kuwaajiri watumishi wa Umma  (PSC) kutilia shaka vyeti vinavyotolewa na taasisi hiyo.

DCI, ilisema uchunguzi wake ulibainisha kuwa Kiyeng alisingizia kuwa taasisi hiyo ya elimu ni mshirika wa Chuo Kikuu ya Moi na hivyo kumhadaa mwathiriwa kujiunga nayo na kusomea stashahada ya usimamizi wa biashara.

Baada ya kukamilisha muda wa somo hilo, mwathiriwa alikabidhiwa cheti cha diploma alichoamini kilikuwa halali na kumkabidhi mwajiri wake kama sehemu ya ufaafu wake kazini.

Hata hivyo baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa cheti hicho kilikuwa bandia, na kusababisha mwathiriwa huyo kuachishwa kazi.

Mshukiwa huyo atafunguliwa mashtaka ya kutenegeneza stakabadhi bandia kinyume na sehemu ya 347(a) ya katiba ya Kenya.

TAGGED:
Share This Article