Masengeli atetea polisi dhidi ya madai ya kutotekeleza sheria kwa usawa

Alisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kutendewa kwa usawa chini ya sheria.

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Gilbert Masengeli, amesisitiza tena dhamira ya Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, ya kutekeleza sheria kwa haki na bila ubaguzi, akieleza kuwa Wakenya wote ni sawa mbele ya sheria.

Akizungumza baada ya kuongoza hafla ya kufunga kambi ya mashindano ya kitaifa ya maskauti wa Kenya mjini Thika, Masengeli alipuuza madai kwamba polisi hutekeleza sheria kwa kuchagua watu wanaowalenga, hasa katika kesi zinazohusisha wanasiasa wanaotuhumiwa kwa kuchochea vurugu.

Alisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kutendewa kwa usawa chini ya sheria na kwamba operesheni za polisi zinaongozwa na misingi ya kisheria na ya Katiba.

Naibu huyo wa Inspekta Jenerali pia alisisitiza azma ya NPS ya kuendelea kukabiliana na magenge ya uhalifu na watu wanaohusika katika vitendo vya vurugu kote nchini.

Alionya kuwa vyombo vya usalama vitaendelea kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wahusika wa kuchochea machafuko na kuvuruga utulivu wa umma.

Masengeli aliwataka vijana wanaoshawishiwa na kuajiriwa na wanasiasa kushiriki vurugu katika mikutano ya kisiasa kuacha na kuelekeza nguvu zao kwa mambo yenye manufaa zaidi.

Aliwahimiza kuzingatia kujiunga na harakati za uskauti, akisema zinawajengea nidhamu, uzalendo, uongozi na hali ya kuwajibika kwa taifa.

Kauli zake zinajiri wakati mjadala wa umma kuhusu kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa viongozi wa kisiasa wanaotuhumiwa kwa uchochezi unaendelea kushika kasi, huku baadhi ya wananchi wakieleza wasiwasi kuhusu iwapo sheria inatekelezwa kwa usawa na bila upendeleo.

Share This Article