Mkuu wa mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ughaibuni, Musalia Mudavadi, amepongeza kuimarika kwa ushirikiano kati ya Kenya na Colombia.
Alisema hayo wakati alikuwa akiaga Balozi wa Colombia nchini Kenya, Pedro León Cortés Ruiz, ambaye amehitimisha muda wake wa utumishi jijini Nairobi.
Mudavadi alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu cha balozi huyo, ushirikiano wa kisiasa umeimarika kwa kiasi kikubwa huku sekta za biashara, uwekezaji, kilimo, uhifadhi wa mazingira, utamaduni na mahusiano kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili zikipanuliwa.
Alisema diplomasia inahusu kujenga mahusiano yanayozalisha fursa kwa wananchi, akibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana yameweka msingi imara wa ushirikiano wa siku zijazo.
Mudavadi alisema Kenya inalenga kupanua ushirikiano na Colombia katika biashara ya pande mbili, ubunifu wa kilimo, uhamishaji wa teknolojia, uongezaji thamani wa bidhaa, utalii, elimu, sayansi na teknolojia, utamaduni na uwekezaji.
Alieleza imani kuwa ushirikiano huo utafungua fursa mpya za ubunifu, ukuaji wa uchumi na ustawi wa pamoja.
Mudavadi alimshukuru Balozi Cortés Ruiz kwa huduma yake ya kujitolea na mchango wake mkubwa katika kuimarisha urafiki kati ya mataifa hayo mawili.