Kalonzo akaribisha Gachagua na Wamalwa kwa mazungumzo

Mkutano huo wa mashauriano unalenga kuimarisha ushirikiano wa vyama vya upinzani.

Marion Bosire
1 Min Read

Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, leo Jumanne Agosti 4, 2026 amewaalika Rigathi Gachagua na Eugine Wamalwa nyumbani kwake.

Kalonzo alisema lengo la mkutano huo na viongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party, DCP na wa chama cha Democratic Action Party Kenya, DAP-K, mtawalia ni kukuza umoja katika upinzani.

Alisema pia kwamba mkutano huo wa mashauriano unalenga kuimarisha ushirikiano wa vyama vya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Kalonzo alisema mkutano huo ni sehemu ya mashauriano yake yanayoendelea na vyama na makundi yenye mtazamo unaofanana, kufuatia mamlaka aliyopewa na Baraza la Pamoja pamoja na Kamati Kuu ya Kitaifa ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ya kuongoza juhudi za kupanua na kuimarisha umoja wa muungano huo.

Viongozi hao watatu walithibitisha tena dhamira yao ya kuendelea na mashauriano, kujenga miungano na kuimarisha ushirikiano kati ya vyama vya upinzani, wakisema lengo lao ni kuwasilisha umoja imara unaoweza kutoa uongozi unaoakisi matarajio ya Wakenya.

Share This Article