Wazee wa vijiji kulipwa shilingi 3,000 kila mwezi

Rais Ruto alisema  wazee hao pia watasajiliwa kwenye Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA), kama juhudi za kuunga mkono mchango wao katika uongozi wa mashinani. 

Tom Mathinji
2 Min Read
William Ruto - Rais wa Kenya.

Rais William Ruto ametangaza kuwa wazee wa vijiji wataanza kupokea marupurupu ya kila mwezi ya shilingi 3,000 kuanzia mwezi Agosti, 2026.

Kiongozi wa taifa alisema hatua hiyo ni katika kutambua jukumu wanalotekeleza wazee hao katika kudumisha amani, kusuluhisha mizozo na kufanikisha utekelezaji wa mipango ya serikali katika kiwango cha mashinani.

“Kuanzia leo, kila mzee wa kijiji atalipwa marupurupu ya shilingi 3,000 kila mwezi,” alisema Rais Ruto.

Akizungumza kwenye mkutano na takriban wazee wa vijiji 10,000 katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema  wazee hao pia watasajiliwa kwenye mpango wa Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA), kama sehemu ya juhudi za kutambua na kuunga mkono mchango wao katika uongozi wa mashinani.

Rais William Ruto akutana na wazee wa vijiji 10,000 katika Ikulu ya Nairobi.

“Kila mzee wa kijiji na familia yake watasajiliwa kwa mpang halmashauri ya SHA, serikali ikilipa mchango unaohitajika,” alisema Rais Ruto.

Wakati huo huo, Ruto aliagiza kuwa wazee hao wa vijiji wapewe vifaa vya mawasiliano ya dijitali na kutoa wito wa kubuniwa kwa sheria zitakazobainisha wajibu wao katika mfumo wa uongozi wa taifa hili.

Aliwataja wazee hao kuwa wahifadhi wa amani, wapatanishi wa mizozo, walinzi wa amali za kijamii na watunzaji wa familia akiongeza kusema kuwa wao ni kiungo muhimu baina ya wananchi na serikali.

Share This Article