Timu ya taifa ya wanawake ya soka Harambee Starlets, imeyaaga mashindano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika kwa Wanawake, WAFCON 2026 bila kuandikisha ushindi wowote.
Wanadada hao wa kocha Beldine Odemba walifungwa mabao 2-0 na Algeria jana Jumatatu usiku kwenye mechi yao ya mwisho ya kundi A iliyochezwa katika uwanja wa Olimpiki wa Rabat.
Mabao hayo yaliyofungwa kwenye kipindi cha kwanza na Marine Dafeur na Lynda Bendris, yameihakikishia Algeria nafasi katika hatua ya robo fainali kwenye mashindano hayo.
Morocco ndio wanaoogoza Kundi A baada ya kutofungana na Senegal katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Prince Moulay El Hassan jijini Rabat.
Starlets wanavuta mkia kwenye kundi A baada ya kupoteza mechi zao zote.
Katika mechi ya kwanza, walifungwa mabao 4-0 na Morocco, mechi ya pili wakapoteza bao 1-0 dhidi ya Senegal na hatimaye wakafungwa na Algeria 2-0.