Mashindano ya shule za Upili: Kakamega, Joga,Chesamisi na Kesogon watwaa mataji

Kufuatia ushindi huo, timu hizo zitashiriki mashindano ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili mjini Morogoro nchini Tanzania baadae mwezi huu.

KBC Digital News
2 Min Read
Kakamega, Joga,Chesamisi na Kesogon watwaa mataji.

Shule ya wavulana ya Kakamega almaarufu kama Green Commandoes leo Alhamisi imenyakua taji la 13 la soka ya kitaifa baina ya shule za upili mjini Thika baada ya ushindi wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya Yala ( Black Saints).

Kwenye mechi hiyo, kakamega ilitangulia kulenga lango katika dakika za mwanzo kisha Yala ikasawazisha baadae. Katika kipindi cha Pili, Yala ilirejea kwa kishindo na kuongeza la pili ila Kakamega ikajibu tena hivyo muda wa kawaida ukaishia magoli mawili kwa mawili.

Kwenye muda wa ziada, Commandoes walivyatua makombora mazito yaliyomwacha hoi mlinda lango wa Black saint hivyo kupata la tatu na la ushindi wa fainali hiyo.

Kwenye ngarambe za vidosho, St.Joseph ya Kitale ( Joga) ilivuna tuzo hilo kupitia mikwaju ya adhabu ya saba kwa sita dhidi ya Nyakach ya Nyanza baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja katika muda wa kawaida na ule wa ziada.

Katika uga wa Voliboli, Chesamisi ya Magharibi ilitawazwa bingwa dhidi ya ACK Chepsaita kwa seti tatu kwa moja za (25–23, 14–25, 25–23, 25–18). Kabla ya hayo, Akina dada wa Kesogon waliwalaza Soweto (Nairobi) seti tatu kwa nunge za 25- 13, 25- 10 na 25-18.

Kufuatia ushindi huo, timu hizo zitashiriki mashindano ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili mjini Morogoro nchini Tanzania baadae mwezi huu.

Share This Article