Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamemkamata Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia Jumatatu asubuhi, kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa eneo la Kieni, kaunti ya Nyeri.
Mbunge huyo alikamatwa baada ya kukesha usiku kucha katika afisi za chumba kimoja cha habari, alikoshiriki mahojiano kwenye moja ya runinga ya kampuni hiyo.
Kaguchia, ambaye ni mwandani wa kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, amekuwa akimulikwa na vyombo vya usalama baada ya kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa siku ya Jumamosi, yanayodaiwa kuwaonya wakazi wa mlima Kenya dhidi ya kumpigia kura Rais William Ruto wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, Kaguchia amekanusha kutoa matamshi ya chuki, akisema alinukuliwa visivyo.
Kukamatwa kwa mbunge huyo kunajiri huku asasi za usalama zikiendelea kuwachunguza baadhi ya wanasiasa wanaodaiwa kutoa matamshi yanayochochea jamii.
Tume ya Mshikamano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC), pia inawachunguza baadhi ya viongozi wa kisiasa akiwemo Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, Waziri wa Afya Aden Duale na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, kwa madai ya kutoa semi za uchochezi.