Watu 8 wafariki kwenye ajali ya barabarani Kirinyaga

Wakazi wa ene hiyo wameitaka Wizara ya Barabara kuharakisha ukarabati wa barabara hiyo kuu na kuweka matuta ya kudhibiti kasi

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu 8 wafariki kwenye ajali ya barabarani Kirinyaga.

Watu wanane wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani katika eneo la Murubara katika  Barabara Kuu ya Mwea-Embu, Kaunti ya Kirinyaga.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, tuk-tuk iliyokuwa ikiwasafirisha wafanyakazi wa shambani katika mradi wa uzalishaji mpunga iligongana ana kwa ana na lori la kubeba mizigo lililokuwa likielekea Embu. Wakazi hao walisema lori hilo lilikuwa likijaribu kuepuka mashimo barabarani.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Mwea Mashariki, Stephen Okal, ambaye alithibitisha ajali hiyo kupitia kwa njia ya simu, alisema watu hao wanane walifariki papo hapo, huku wengine watatu, akiwemo dereva wa lori, wakipata majeraha madogo na kupelekwa  katika Hospitali ya matibabu maalum ya Kerugoya Level Five.

Miili ya wanane hao ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Level 5 ya Kerugoya.

Kutokana na ajali hiyo, wakazi wa ene hiyo wameitaka Wizara ya Barabara kuharakisha ukarabati wa barabara hiyo kuu na kuweka matuta ya kudhibiti kasi katika sehemu zinazoweza kusababisha ajali ili kuzuia maafa  zaidi.

Share This Article