Mwanamuziki wa Kenya Akothee amerejea nchini kwa ajili ya tamasha inayosubiriwa kwa hamu ya Nadia Mukami@10, ambapo alipokelewa kwa uchangamfu katika Uwanja wa Ndege na Nadia Mukami mwenyewe.
Muda mfupi baada ya kuwasili, Akothee alitumia mitandao ya kijamii kutoa wito wa wasanii wa kike kupatiwa uungwaji mkono, akisema kuwa wanawake wengi wenye vipaji katika sekta ya muziki bado wanapuuzwa.
Alisema kuwa watu mashuhuri mara nyingi huwachangamkia na kusherehekea wasanii wa kimataifa badala ya kuinua vipaji vya nyumbani, akiongeza kuwa hali hiyo imekwamisha maendeleo ya wanawake katika muziki.
Akothee pia alilinganisha Kenya na mataifa kama Nigeria, Tanzania na Uganda, ambako alisema wanamuziki hupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wasanii wenzao, vyombo vya habari na wananchi.
Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, wasanii wa kike nchini Kenya mara nyingi hukumbana na ukosoaji na mashambulizi ya kibinafsi kila wanapotoa nyimbo mpya badala ya kutiwa moyo na kuungwa mkono.
Akothee aliwasihi Wakenya kuwapa wasanii wa kike heshima wanayostahili kupitia kupigwa kwa nyimbo zao hewani, kuwapa nafasi za kutumbuiza na kuwaunga mkono kwa dhati.
“Kuna nafasi ya kila mwanamke kung’ara. Kumuunga mkono mwanamke mwingine mwenye kipaji hakupunguzi mwanga wako. Tutasapotiana hadi tuvunjike,” Akothee aliandika.
Nadia anaadhimisha miaka 10 katika tasnia ya muziki ambapo ameandaa tamasha Nairobi Agosti Mosi, 2026.