Gavana wa zamani wa kaunti ya Migori Zachary Okoth Obado na washtakiwa wenzake wawili wamekutwa na hatia katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.
Uamuzi kuhusu kesi hiyo iliyofuatiliwa sana na umma, umetolewa leo na Jaji wa Mahakama Kuu Cecilia Githua.
Jaji alisema mahakama ilipata kwamba ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha pasi na shaka kwamba watatu hao pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani walishirikiana katika kutekeleza uovu huo.
Mshatakiwa wa kwanza Obado analaumiwa kwa kuja na wazo la uovu huo, mshtakiwa wa pili Michael Oyamo akawezesha utekelezaji na mshtakiwa wa tatu Casper Ojwang akatoa usaidizi katika utekelezaji huo.
Kulingana na Mahakama, kutokuwepo kwa mshtakiwa wa kwanza binafsi katika eneo la tukio siku hiyo, hakumpi ulinzi dhidi ya wajibu katika kesi hiyo ya jinai.
Jaji Githua alisema kwamba wajibu wa jinai hautegemei eneo ambalo watu walio na nia moja wapo.
Mahakama ilihitimisha kwamba mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu ni wahalifu wakuu kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Kanuni ya Adhabu.
“Kwa kuzingatia ushahidi wa mazingira, washtakiwa hao walisababisha moja kwa moja kifo cha marehemu wakiwa na nia mbaya ya awali,” alisema Jaji huyo.
Aliongeza kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake dhidi ya kila mmoja wa washtakiwa na hivyo, kila mmoja wao ana hatia kwa kosa hilo kama lilivyo katika hati ya mashtaka.