Wakazi Kigali kufurahia muziki wa Afrika Mashariki wikendi hii

Awamu ya tatu ya tamasha ya 'Tunataka Ku Enjoy' itaandaliwa katika kituo cha Mundi Julai 25 na 26, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Wakazi wa Kigali wanatarajiwa kufurahia wikendi yenye burudani ya kipekee katika awamu ya tatu ya Tamasha ya ‘Tunataka Ku Enjoy’ wikendi hii.

Tamasha hiyo itafanyika katika kituo cha Mundi Julai 25 na 26, 2026 likiwakutanisha wasanii mashuhuri wa muziki kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

Tamasha hiyo, inayoandaliwa na Hottempah Collective ni ya siku mbili na itawakutanisha wasanii kutoka Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Burundi.

Itaonyesha utofauti mkubwa wa muziki wa ukanda huu kupitia maonyesho ya moja kwa moja, burudani za wapiga muziki yaani DJss na shughuli mbalimbali za kitamaduni.

Wasanii watakaotumbuiza ni pamoja na Azawi kutoka Uganda, Kirikou Akili kutoka Burundi, DJ Mkuzi kutoka Tanzania, Mista C kutoka Kenya na Christopher, Nel Ngabo, Mike Kayihura, Ish Kevin, Davis D, Angell Mutoni, DJ Lamper na Starving Yet Full kutoka Rwanda.

Waandaaji wa tamasha hiyo wanasema lengo ni kuendeleza vipaji vya wasanii wa Afrika Mashariki huku ikiwapa watazamaji fursa ya kufahamu wasanii kutoka nchi jirani.

Mbali na muziki, washiriki watapata fursa ya kufurahia vyakula kutoka kwa wauzaji mbalimbali, maonyesho ya mitindo na bidhaa za maisha, michezo na shughuli za kijamii zitakazofanyika katika majukwaa matatu ya Silver, Gold na Mist.

Wasanii wakuu watatumbuiza kwenye jukwaa la Gold kuanzia saa moja usiku hadi usiku wa manane, huku burudani za Afro House, Amapiano na 3-Step zikiendelea katika jukwaa la Mist hadi saa nane usiku.

Share This Article