Serikali yarejelea msako dhidi ya Shisha

Katibu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema kuwa serikali ina wasiwasi kwamba inachangia magonjwa ya pumu.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali imerejelea msako dhidi ya sigara za kielektroniki na shisha, kutokana na wasiwasi kuhusu mchango wake katika ongezeko la magonjwa ya mfumo wa kupumua nchini.

Katibu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema kuwa serikali ina wasiwasi kwamba bidhaa nyingi zinaingizwa nchini Kenya kimagendo kupitia nchi jirani kwa ajili ya majaribio na matumizi, kinyume na sheria na kanuni zilizopo.

Katibu huyo alizungumza mjini Thika, Kaunti ya Kiambu, wakati wa ukaguzi wa zaidi ya pakiti 17,000 za sigara zinazoshukiwa kuwa bandia ambazo zilipatikana katika boma moja eneo hilo.

Alihimiza wazalishaji na waagizaji wa sigara kutanguliza afya ya umma kwa kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingizwa sokoni zinazingatia viwango vya usalama na masharti ya udhibiti vilivyowekwa nchini.

Uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kubaini uhalisi wa sigara hizo na kuwabaini waliohusika katika usambazaji wake.

Muthoni aliwaambia waandishi wa habari kuwa bidhaa hizo zitaharibiwa iwapo vipimo vitathibitisha kuwa ni bandia.

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini, KRA pia imeanzisha uchunguzi wa sambamba ili kubaini iwapo mzigo huo ulizingatia masharti ya forodha, kama kulipa kodi zinazostahili na uwekaji wa stempu za lazima za ushuru wa bidhaa.

Share This Article