Mwanamuziki wa kike wa Uganda Kapa Cat amezua gumzo nchini humo baada yake kutoa maoni ya kudunisha tasnia ya muziki nchini humo akisema wanamuziki wa sasa wa Uganda wanachosha na hawana ubunifu.
Akizungumza kwenye mahojiano, mrembo huyo aliunga mkono kauli za hivi karibuni za Jowy Landa, akisema kuwa muziki wa sasa umekuwa wa kutabirika na hauna mambo mapya ya kuvutia mashabiki.
Kapa Cat alifichua kuwa mara kadhaa amewasiliana na baadhi ya wanamuziki wa kike akipendekeza mashindano ya kirafiki ya muziki ili kuongeza msisimko na burudani kwa mashabiki.
Kulingana naye, wengi wao wamekataa wazo hilo kwa sababu wanaogopa kushindana.
Kapa alisisitiza kuwa yuko tayari kukabiliana na msanii yeyote wa kike katika mashindano ya kirafiki ya uwezo wa kuandika na kuimba nyimbo endapo fursa hiyo itajitokeza.
Alipoulizwa kuhusu wanamuziki wa kiume, Kapa Cat alisema kuwa Peter Miles ndiye msanii pekee ambaye anaamini anaweza kushindana naye kwa urahisi.
Kauli zake zinakuja wakati ambapo mashabiki wengi pamoja na wadau wa tasnia ya muziki wanadai kuwa muziki wa Uganda umedorora, huku nyimbo chache mpya zikifanikiwa kuacha alama ya kudumu.
Baadhi wanaamini kuwa nyimbo zinazotawala kwa sasa kwenye orodha ni zile za zamani, jambo linalochochea wito kwa wasanii kufufua ushindani uliowahi kushamiri enzi za ushindani mkubwa kati ya Bebe Cool, Jose Chameleone na Bobi Wine, ambao wengi wanaamini uliifanya tasnia ya muziki kuwa hai na kuvutia umma.