Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi meli nne za kubeba mizigo katika Bandari ya Kigoma, hatua inayolenga kuimarisha usafirishaji wa mizigo katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Kulingana na Rais huyo, mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya uchukuzi na kuongeza ufanisi wa huduma za bandari ili kuchochea biashara na ukuaji uchumi.
Kwenye taarifa aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa X siku ya Jumatatu, Samia alidokeza kuwa meli hizo zinatarajiwa kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo ndani na nje ya Tanzania kupitia Ziwa Tanganyika, huku zikirahisisha shughuli za kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani zinazotumia ziwa hilo, ikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.
Mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na unatarajiwa kuimarisha nafasi ya Bandari ya Kigoma kama kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Kwenye ziara yake katika eneo la Kigoma, Rais Samia pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha reli ya kisasa (SGR), yenye urefu wa kilomita 506.
Alisema serikali yake inaendelea kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi unaounganisha reli, bandari, barabara na viwanja vya ndege ili kupunguza gharama ya usafirishaji, kuongeza ushindani wa kibiashara na kufungua masoko mapya.