Rais William Ruto amempongeza Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Andy Burnham, akimtakia ufanisi anapoanza kutekeleza rasmi majukumu yake.
Amesema kuteuliwa kwa Burnham kunatokana na rekodi yake njema ya uongozi na uzingatiaji wa maadili ambayo yanawiana na ajenda ya Kenya ya kuimarisha uchumi kutoka chini hadi juu, almaarufu Bottom up.
“Kwa niaba ya watu wa Kenya, nakutakia ufanisi kwenye majukumu yako,” alisema Rais Ruto kupitia ukurasa wa X siku ya Jumatatu.
Aliongeza kuwa anatazamia kushirikiana na Waziri Mkuu huyo kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili na kupanua ushirikiano katika biashara na uwekezaji, ukuaji wa nishati safi, uvumbuzi na usalama miongoni mwa masuala mengine.
“Pamoja tutaimarisha urafiki kati ya nchi hizi na kubuni fursa pana na ufanisi wa pamoja kwa raia wa nchi hizo,” alisema Rais.
Andy Burnham amechukua rasmi wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza baada ya Mfalme Charles III kumwalika kuunda serikali katika mkutano wa faragha uliofanyika katika Kasri ya Buckingham.
Burnham ni Waziri Mkuu wa 59 wa Uingereza na alichukua wadhifa huo baada ya kujiuzulu kwa Keir Starmer.