Fik Fameica kusherehekea miaka 10 ya muziki

Tamasha hiyo huenda ikafanyika mwezi Desemba 2026 au Januari 2027.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Fik Fameica amefichua kwamba tamasha lake kubwa lijalo litakuwa hatua muhimu katika safari yake ya muziki, akijiandaa kuadhimisha miaka 10 katika tasnia ya muziki nchini Uganda.

Msanii huyo amesema tayari ameanza kufanya maandalizi ya tamasha hilo na atatoa tangazo rasmi hivi karibuni.

Fik, ambaye tamasha lake la mwisho lilifanikiwa mwezi Septemba mwaka jana, amesema ameona ongezeko la mashabiki wanaouliza kuhusu siku atarejea jukwaani.

Kwa mujibu wa rapa huyo, aliamua kwa makusudi kuchukua muda kabla ya kuandaa tamasha jingine ili aweze kuwapa mashabiki wake burudani kubwa na bora zaidi kuliko alivyowahi kufanya hapo awali.

“Nimekuwa nikiona maombi kutoka kwa mashabiki wangu kwenye mitandao ya kijamii. Nafikiri tamasha langu lijalo linapaswa kuwa la kuadhimisha miaka 10 katika tasnia ya muziki. Nilitaka kujipa muda ili niweze kufanya jambo bora zaidi kuliko yale niliyowahi kufanya.” Alisema.

Fameica ameongeza kuwa tamasha hilo la maadhimisho huenda likafanyika mwezi Desemba 2026 au Januari 2027.

Mashabiki wanatarajiwa kupata taarifa zaidi katika miezi ijayo huku maandalizi ya maadhimisho hayo muhimu yakiendelea kushika kasi.

Fameica ambaye jina lake halisi ni Shafik Walukagga, wa umri wa miaka 30 alianza kazi kama mwanamuziki mwaka 2015 na ameendelea kukua katika tasnia hiyo hadi sasa.

Share This Article