Serikali ya Kenya Kwanza imedhamiria kuendelea kuwahudumia Wakenya kwa uwazi, uwajibikaji, upatikanaji mkubwa wa taarifa na mabadiliko endelevu ya kidijitali.
Rais William Ruto ametaja uwazi kuwa kiungo muhimu cha kupata uaminifu wa umma katika utendaji kazi wa serikali.
“Duniani kote, uaminifu katika taasisi za umma unakumbwa na shinikizo linaloongezeka. Teknolojia imepanua utapatikaji wa taarifa, lakini pia imeongeza upotoshaji wa taarifa, uongo na maudhui yaliyotiwa chumvi. Matokeo yake ni kwamba wananchi wanaiuliza serikali maswali magumu, na wako sawa kufanya hivyo. Uaminifu hauwezi tu kudaiwa, unapaswa kutafutwa,” alisema Rais Ruto.
“Na njia bora zaidi ya kutafuta uaminifu huo ni kupitia uwazi. Wananchi wanaweza wakaamini zaidi taasisi za umma wakati wanapoelewa namna maamuzi yanavyofanywa, namna rasilimali zinavyosimamiwa, na namna serikali inavyoshughulikia mahitaji yao.”
Rais Ruto aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Kitaifa ya Uwazi ya kwanza itakayokuwa ikitolewa kila mwaka ikiangazia uwazi serikalini, ikiwa ni pamoja na katika wizara, idara, mashirika, tume za kikatiba na serikali za kaunti.
Ruto pia ametoa wito kwa mashirika ya kijamii, vyuo, vyombo vya habari na kila Mkenya kushiriki mchakato huo wa kutathmini uwazi katika taasisi hizo ili kukuza maongozi bora nchini.
Ripoti hiyo itakuwa ikitayarishwa na Tume ya Utawala wa Sheria, CAJ.