Mbivu na mbichi kujulikana Ol Kalou Alhamisi

Wanaopigiwa upatu kushinda kiti hicho ni ama mgombea wa UDA Muchina Nyagah au Sammy Ngotho wa chama cha DCP chake Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.

Martin Mwanje
3 Min Read

Wakazi wa Ol Kalou wataelekea debeni kesho Alhamisi kumchagua mbunge wao mpya katika uchaguzi mdogo ambao umekumbwa na madai ya kila aina ikiwa ni pamoja na kuwahonga wapiga kura na kuchochea vurugu. 

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na kisha kufungwa saa kumi na moja jioni.

“Ili kupiga kura, ni lazima uwe na kitambulisho chako halisi cha kitaifa au pasipoti halali ya Kenya katika kituo chako cha kupigia kura,” imesema IEBC saa chache kabla ya wakazi wa Ol Kalou kupiga kura.

“Muda wowote uliopotea wakati wa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura utafidiwa wakati wa kufunga vituo hivyo. Wapiga kura wote walio kwenye foleni kufikia saa kumi na moja jioni wataruhusiwa kupiga kura.”

Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ameashiria kuwa hakuna mwanasiasa, haijalishi ni mwandamizi kiasi gani, ataruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura na mawakala au wafuasi ambao hawajaidhinishwa na tume hiyo.

Lengo ni kuhakikisha hakuna vurugu zitatokea na hivyo kutatiza mchakato wa kupiga kura.

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kwa upande wake ameashiria kuwa amewatuma maafisa zaidi ya 1,000 kuhakikisha usalama wa kutosha wakati na baada ya kupiga kura.

Kanja ameonya kuwa yeyote atakayepatikana akivunja sheria atajutia matendo yake.

Eneo bunge la Ol kalou lina wapiga kura 73,480 na vituo 144 vya kupigia kura.

Ushindani mkuu hasa ni kati ya mgombea wa chama tawala cha UDA Muchina Nyagah na Sammy Ngotho wa chama cha DCP.

Uchaguzi huo unatumiwa kupima ubabe wa kisiasa kati ya Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na mtangulizi wake Rigathi Gachagua katika eneo la Mlima Kenya.

Ingawa Gachagua anadai chama cha UDA kimepoteza ubabe wake wa kisiasa katika eneo hilo baada ya yeye kutimuliwa serikalini, chama cha UDA kinashikilia kuwa bado kina usemi wa kisiasa katika eneo hilo kama ilivyodhihirika katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini.

Ikiwa UDA itashinda tena uchaguzi mdogo wa hiyo kesho, basi dhana hiyo huenda ikapata mashiko zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou unaandaliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mjumbe wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mapema mwaka huu.

 

Share This Article