Mikel Oyarzabal na Pedro Porro walibusu nyavu mara moja kila mmoja na kuisaidia Uhispania kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia, baada ya kuitema nje Ufaransa kwa ushindi wa mabao 2-0 katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Jumanne usiku uwanjani Dallas, Marekani.
La Roja walikata mashambulizi yote ya Ufaransa ambao kabla ya nusu fainali, walikuwa timu yenye ufungaji bora kwenye kipute hicho, huku Oyarzabal akipachika bao la kwanza kupitia penalti baada ya Lamine Yamal kuangushwa na Lucas Digne.
Kipindi cha pili, Uhispania waliendelea kumiliki mpira na kujihami na Wafaransa wakifanya shambulizi walijikuta kwenye njia panda baada ya kujisahau na kumruhusu Porro kupachika bao lingine lililozamisha matumaini yao.
Uhispania walifanikiwa kushinda Ufaransa kwa mara ya 37 na kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili, baada ya subira ya miaka 16 walipotwaa ubingwa nchini Afrika Kusini.
Uhispania sasa watachuana na aidha Uingereza au Argentina katika fainali Jumapili hii mjini New York.