Rais Ruto amwomboleza Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani

Rais alitoa pole kwa niaba yake binafsi pamoja na kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametuma salamu za rambirambi za dhati kutoka Kenya kufuatia kifo cha Baba Amir, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, babake kiongozi wa Qatar, Amir Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.

Katika ujumbe wake wa rambirambi, Rais Ruto amesema amehuzunishwa sana na kifo cha kiongozi huyo mashuhuri wa Qatar na kutoa pole kwa niaba yake binafsi pamoja na kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kenya.

Rais alitoa rambirambi zake za dhati kwa Amir Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, familia ya Al Thani, pamoja na Serikali na wananchi wa Taifa la Qatar katika kipindi hiki cha maombolezo.

Rais Ruto alimtaja marehemu Baba Amir kuwa kiongozi aliyekuwa na maono aliyeongoza Qatar katika kipindi cha maendeleo makubwa na ustawi wa kiuchumi, huku akiweka misingi ya Qatar ya kisasa.

Alisema kujitolea kwake, busara na maono yake viliibadilisha nchi hiyo na kuacha urithi wa kudumu ambao utaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo.

Kiongozi wa Taifa alisema Kenya iko pamoja na wananchi wa Qatar katika kipindi hiki cha majonzi kufuatia kuondokewa na kiongozi aliyekuwa akiheshimika, ambaye mchango wake ulihisiwa sio tu nchini Qatar pekee bali pia katika jumuiya ya kimataifa.

Rais Ruto pia aliombea roho ya marehemu Baba Amir ipumzike kwa amani na akamwombea Amir Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, familia ya Al Thani, pamoja na wananchi wa Qatar wapate nguvu, faraja na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

Share This Article