Rais Ruto apongeza timu ya Junior Starlets

Timu hiyo imefuzu kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la Wasichana Chini ya Miaka 17 mwaka 2026.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais William Ruto akutana na viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Marsabit katika Ikulu ya Nairobi.

Rais William Ruto ameipongeza timu ya taifa ya wasichana wa umri wa chini ya miaka 17, Junior Starlets kwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la Wasichana Chini ya Miaka 17 mwaka 2026.

Alitaja hatua hiyo kuwa ya mafanikio na muhimu katika historia ya soka ya Kenya.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya Kenya kuishinda Afrika Kusini, Rais Ruto alisema mafanikio ya timu hiyo yanaonyesha uwezo wa Kenya kufanya vyema kimataifa na ni chanzo cha hamasa kwa wanamichezo vijana kote nchini.

“Tunajivunia sana Junior Harambee Starlets wetu kwa kufuzu kwao kwa kihistoria kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la Wasichana Chini ya Miaka 17 mwaka 2026,” alisema Ruto.

Alisema wachezaji hao wa umri mdogo wameliweka taifa karibu zaidi na ndoto ya kushindana katika jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.

Aliongeza kuwa mafanikio ya Junior Harambee Starlets yatahamasisha kizazi kipya cha wanamichezo wa kike na wa kiume kufuatilia ndoto zao kwa ujasiri na azma, wakiamini kwamba hakuna ndoto isiyoweza kutimizwa.

“Nawapongeza wachezaji, benchi la ufundi, Shirikisho la Soka Kenya, FKF na kila Mkenya aliyesimama pamoja na timu hii. Hongera, Junior Harambee Starlets. Nyinyi ni mashujaa,” alisema Ruto.

Junior Harambee Starlets walijihakikishia nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la Wasichana Chini ya Miaka 17 mwaka 2026 baada ya kuiondoa Afrika Kusini katika mechi za kufuzu, na hivyo kuwa miongoni mwa wawakilishi wa Afrika katika mashindano hayo ya dunia.

Share This Article