Bei za mafuta zaongezeka duniani

Hali hii inatokana na kurejelewa kwa mapigano ya kijeshi kati ya Marekani na Iran.

Marion Bosire
2 Min Read

Bei za mafuta duniani zilipanda kwa kasi leo Jumatatu kufuatia kurejelewa kwa mapigano ya kijeshi kati ya Marekani na Iran.

Hali hiyo imeongeza hofu ya usumbufu katika usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu kwa usambazaji wa nishati duniani.

Mafuta ghafi aina ya Brent, ambayo ni kipimo cha kimataifa cha bei ya mafuta, yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia nne na kufikia dola 79.26 kwa pipa, kiwango cha juu zaidi tangu Juni 22, huku wawekezaji wakijibu kuongezeka kwa mapigano.

Ongezeko hilo lilifuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani yaliyolenga maeneo ya Iran baada ya Washington kuishutumu Tehran kwa kushambulia meli ya kibiashara iliyokuwa ikipita katika njia hiyo muhimu ya baharini.

Kujibu mashambulizi hayo, Iran ilirusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea mataifa kadhaa ya Ghuba, kama Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, ikionya kuwa meli zitakazotumia njia zisizotambuliwa na mamlaka zake hazitapatiwa dhamana ya kupita salama.

Shughuli za usafirishaji wa meli kupitia Mlango wa Hormuz zimepungua kwa kiasi kikubwa tangu mapigano mapya yaanze na kuzua wasiwasi kuhusu usumbufu wa usambazaji wa mafuta kupitia njia inayobeba takriban asilimia 20 ya biashara ya mafuta duniani.

Mvutano huo mpya pia uliyumbisha masoko ya fedha, huku hisa nchini Japan na Korea Kusini zikishuka kwa kiwango kikubwa kutokana na tahadhari inayoongezeka miongoni mwa wawekezaji.

Share This Article