Kocha wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Benni McCarthy amekitaja kikosi cha awali kwa mechi mbili zijazo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Gambia na Gabon.
McCarthy aliyetambulishwa wiki jana amewajumuisha chipukizi na wachezaji wenye tajiriba katika timu hiyo.
Harambee Stars watamenyana na Gambia Machi 20 mjini Abidjan, Ivory Coast, kabla ya kuwaalika Gabon siku nne baadaye katika mechi za tano na sita kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka ujao.
McCarthy amewaita kikosini Edward Omondi, Ben Stanley, Kelly Madada, na Andreas Odhiambo sawia na kiungo mzaliwa wa Australia William Lenkupae.
Nahodha Michael Olunga, atashirikiana katika safu ya mashambulizi inayowajumuisha pia Jonah Ayunga na Masud Juma.
Safu ya nyuma inawajumuisha Joseph Okumu wa Reims ya Ufaransa, Daniel Anyembe wa Viborg FF ya Uswidi, na Brian Mandela wa Stellenbosch ya Afrika Kusini.
Richard Odada, Duke Abuya, na Timothy Ouma ni baadhi ya mihimili ya kiungo cha kati.
McCarthy ametangaza kuwa na kambi ya wachezaji nyumbani kuanzia tarehe 12 mwezi huu ili kuwapiga msasa kwa kipute cha fainali za kombe la CHAN.
Kikosi kamili
Makipa: Brian Opondo (Tusker FC), Faruk Shikhalo (Bandari FC), Ian Otieno (Richards Bay, South Africa), Brian Bwire (Polokwane City, South Africa)
Mabeki: Sylvester Owino (Gor Mahia), Ronney Onyango (Gor Mahia), Alphonce Omija (Gor Mahia), Siraj Mohamed (Bandari FC), Daniel Sakari (Kenya Police FC), Levis Esambe (AFC Leopards SC), Eric Ouma (Rakow Czestochowa, Poland), Johnstone Omurwa (Kapaz FC, Azerbaijan), Joseph Okumu (Stade Reims, France), Collins Sichenje (FK Vojvodina, Serbia), Daniel Anyembe (Viborg FF, Denmark), Brian Mandela (Stellenbosch, South Africa), Amos Nondi (Ararat, Armenia)
Kiungo: Brian Musa (Kenya Police FC), Chris Erambo (Tusker FC), Austine Odhiambo (Gor Mahia), Lawrence Juma (Gor Mahia), Kelly Madada (AFC Leopards SC), Ben Stanley (Gor Mahia), Mathias Isogoli (KCB FC), Andreas Odhiambo (Kariobangi Sharks), Alpha Onyango (Gor Mahia), Richard Odada (OFK Beograd, Serbia), Duke Abuya (Young Africans, Tanzania), Timothy Ouma (Slavia Prague, Czech Republic), Apollo Otieno (Dodoma Jiji, Tanzania), Amos Nondi (FC Ararat, Armenia), Eric Johanna (UTA Arad, Romania), Anthony Akumu (Kheybar Khorramabad, Iran), Ismail Gonzalez (Merida AD, Spain), William Lenkupae (Central Coast Mariners, Australia)
Washambulizi: Boniface Muchiri (Ulinzi Stars), James Kinyanjui (KCB FC), Alvin Mang’eni (Kenya Police FC), Mohamed Bajaber (Kenya Police FC), Eric Balecho (Tusker FC), Ryan Ogam (Tusker FC), Moses Shumah (Kakamega Homeboyz), Edward Omondi (Sofapaka FC), Elvis Rupia (Singida Blackstars, Tanzania), John Avire (Porto Suez, Egypt), Jonah Ayunga (St Mirren, Scotland), Michael Olunga (Al-Duhail, Qatar), Mathew Tegisi (Pamba Jiji, Tanzania), Masud Juma (Esteghlal FC, Iran).
Kenya ni ya nne katika kundi F la kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka ujao kwa alama 5 baada ya kutoka sare mbili kushinda mechi moja na kupoteza moja.